Dibaji

 

Kiikizu, pamoja na lahaja yake Kisizaki, ni lugha katika eneo la Mashariki la lugha za Kibantu. Kinazungumzwa na watu mnamo 55,000 wanaoishi katika mkoa wa Mara wa Tanzania kwa upande wa Kusini wa Wazanaki. Wengi wa Waikizu na Wasizaki wanaishi katika tarafa ya Chamriho, wilaya ya Bunda, mkoani mwa Mara.

 

Kiikizu kinaainishwa katika Ethnologue kuwa lugha ya Niger-Congo, Atlantic-Congo, Volta-Congo, Benue-Congo, Bantoid, Southern, Narrow Bantu, Central, J, Logooli-Kuria (E.402). Waikizu wanaita lugha yao "Ikiikiizʉ" na katika Kiingereza kinaitwa "Ikizu." Maneno ya Kiikizu yanafanana na lugha mbili zingine kwa asilimia kubwa: lahaja Kisizaki (95%) na Kizanaki (87%).